Monday, January 18, 2010

Kwikwi husababishwa na nini?


Baada ya kusoma makala inayohusu kijana mmoja aliyesumbuliwa na kwikwi kwa zaidi ya miaka miwili na nusu, na baadaye kutibiwa tatizo hilo kwa kufanyiwa upasuaji wa ubongo na kutolewa tezi, nimeamua leo nizungumzie kwikwi.
Kwiki ni kitendo kisichozuilika ambacho hutokana na kusinyaa kwa kuta za kiwambo cha moyo au diaphragm. Kwa kawaida kwikwi ni kitendo kinachojirudia rudia mara nyingi. Sauti ya 'hic' inayotokea wakati unapokuwa na kwikwi husababishwa na kidaka tonge (epiglottis) ambacho hufunga haraka wakati hewa inapoingia kwenye koo. Kupiga kwikwi kwa kawaida hakuna maumivu lakini mara nyingine husumbua hasa inapoendelea kwa muda mrefu. Kwikwi ya kawaida huweza kutulizwa kwa kunywa maji, lakini wakati mwingine kufanya hivyo hakusaidii.
Zifutazo ni sababu zinazoweza kukuletea kwikwi
1. Kula kwa haraka.
2. Kula chakula cha moto na kunywa maji baridi baada yake.
3. Kulia au kukasirika.
4. Kula chakula chenye viungo vingi au pilipili.
5. Kula chakula cha moto sana.
6. Kunywa pombe au soda kwa wingi.
7. Kukohoa sana.
8. Kucheka kupita kiasi.
9. Kufurahi sana, kusisimka au kupatwa na msituko.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, vitu ambavyo vinakiletea karaha kiwambo cha moyo au diaphragm husababisha kwikwi. Kuna sababu nyingi ambazo husababisha jambo hilo na hizo tulizotaja hapo juu ni miongoni mwazo,ambapo matokeo yake ni humfanya mtu apige kwikwi. Kwikwi kwa kawaida huisha baada ya dakika chache au hata sekunde. Lakini iwapo kwikwi itaendelea kwa masaa au kwa siku, huweza kuwa ni tatizo muhimu la kitiba na pengine hali kama hiyo inaweza ikawa inasababiswa na ugonjwa.
Kuna baadhi ya watu hupata kwikwi sana wakati wa ujauzito, baada ya kufanyiwa operesheni na hata watoto wachanga pia hupatwa na kwikwi mara kwa mara. Wajawazito hupata kwikwi sana mwishoni mwa miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito na mwanzoni mwa miezi mitatu ya pili. Kwikwi hutokea wakati wa ujauzito ni kwa sababu wakati huo uwezo wa kuvuta hewa ndani ya mapafu na kutoa nje huongezeka kwa asilimia 30 hadi 40 ikilinganishwa na hali ya kawaida. Hakuna sababu inayojulikana inayosababisha kwikwi kwa watoto wachanga, na wazazi wanashauriwa wasitiwe hofu na suala hilo. Hii ni katika hali ambayo kwikwi baada ya upasuaji husababishwa na nusu kaputi au anesthesia.

No comments: