Monday, January 11, 2010

Operesheni ya kwanza duniani ya moyo kwa kutumia MRI yafanywa Uingereza


Mtoto wa kiume wa miaka 6 nchini Uingereza amekuwa mtu wa kwanza duniani, kufanyiwa operesheni ya kupanua chemba ya moyo kwa kutumia muongozo wa MRI badala ya kutumia taswira ya X-ray. Jack Walborn alizaliwa na tatizo la moyo linalojulikana kama Pulmonary Valve Stenosis, hali ambayo huzuia damu kuingia katika mapafu. Kwa kutumia MRI, kunamaanisha kwamb wagonjwa hawatakuwa tena na haja ya kupigwa miale ya X- ray, hasa watoto wadogo. MRI pia inaonyesha taswira nzuri zaidi na kutoa taarifa kuhusiana na tishu za mwili wakati huo huo wa upasuaji. Mtoto Jack alikuwa na tatizo ambalo, damu iliyotoka upande wa kulia wa moyo wake haikuweza kuzunguka. Madaktari wa upasuaji waliamua kuwa, mtoto huyo anahitajia operesheni inayoitwa "valvuloplastry" ili kupanua chemba ya moyo na kuongeza mzunguzuko wa damu. Suala hilo hufanyika kwa kuingizwa mrija au katheta (catheter) katika mshipa wa damu kwenye mkono na kuuisukuma tararibu mrija huo au kuuongoza hadi kwenye moyo. Katika ncha ya mrija huo hufungwa puto ambalo hujazwa hewa ili kupanua chemba ya sehemu hiyo ya moyo iliyo nyembamba. Kwa kawaida X-ray hutumiwa kuangalia na kuongoza harakati ya katheta katika mwili. Lakini timu ya wataalmu wa Afya wa London imegundua njia ya kutumia MRI badala ya X-ray, na upasuaji wa kijana huyo mdogo unaonekana kuwa ni mafanikio makubwa katika uwanja huo. Baada ya kumalizika opersheni hiyo, baadaye Jack alipotoka chumba cha upasuaji alikuwa akikimbia huko na huko na kujisikia vyema. Wataalamu wanasema kwamba, teknolojia hiyo ni mafanikio makubwa, na katika mustaqbali wanataraji wagonjwa wengi wengine watafaidika kwa kutumia MRI badala ya X-ray, na kuepuka kupigwa miale kwani MRI haiumii miale.

No comments: