Sunday, January 3, 2010

Gundua siri ya kulala fofofo


UKOSEFU wa usingizi ni tatizo linalowasumbua wengi maishani, na inakisiwa kuwa zaidi ya humusi ya watu wazima wamewahi kutatizwa na usingizi wakati mmoja maishani mwao.
Ukosefu wa usingizi hutatiza sana , hasa ikiwa utatokea usiku, na mwathiriwa kuhisi usingizi na uchovu mchana, wakati ambapo anafaa kuwa akifanya kazi.
Kuna baadhi ambao, licha ya kulala masaa mengi, miili yao huhisi kwamba haijapata usingizi wa kutosha. Hii mara nyingi hutokana na kutoweza kupata usingizi haraka, kuamka mapema sana au kuwa na usingizi unaotatizika, au usio na raha.
Hii mara nyingi hutokana na mfadhaiko, hamu au wasiwasi kuhusu jambo fulani, hisia pamoja na mazingira kwa mfano kelele, hali ya kitanda au hata watu walio karibu wakati wa kulala.
Kufanya kazi kwa zamu, kwa mfano wakati mwingine usiku na mwingine mchana huwa pia sababu ya matatizo ya usingizi kwa kuwa mwili hushindwa kuzoea. Kufanya kazi zaidi, kunywa pombe kupindukia au hata kunywa vinywaji vyenye viwango vya juu vya kemikali aina ya kafeine ambayo hupatikana kwenye kahawa kadhalika huweza kusababisha matatizo haya.
Matatizo ya mwili kwa mfano majeraha, tatizo la maumbile kama vile kusikia kelele ndani ya sikio tatizo ambalo hujulikana kitaalamu kama tinnitus aidha huweza kutatiza usingizi wa mwanadamu.
Ukiweza kutambua kwa ufasaha kiini cha matatizo yako ya usingizi, unaweza kutafuta suluhisho. Kwa mfano, ikiwa kitanda kiko katika hali mbaya, unaweza kutafuta kingine, au hata kununua godoro na blanketi mpya.
Kuwa na mtindo wa kulala kadhalika husaidia sana . Unafaa kuwa na masaa fulani ya kulala na kuamka ili mwili uzoee.
Ubongo utakuwa tayari kila wakati huo ukifika kupumzisha mwili, na baadaye kuuamsha katika muda ufaao.
Unaweza kualika usingizi kwa kutojishughulisha na mambo mengi wakati wa kulala unapokaribia, kuoga kwa maji moto kiasi au kusikiliza nyimbo tamu. Si ajabu kwamba mama anapotaka mtoto alale, humwimbia nyimbo tamu, na hii hufanikiwa na hata mtoto aliyekuwa akilia akiwa amejawa na hasira hatimaye hulala.
Jiepushe pia na unywaji wa pombe kupindukia, au kunywa vinywaji vyenye viwango vya juu vya kafeine. Ikiwa tatizo lako ni mfadhaiko, tafuta mtaalamu wa matatizo ya fikira au mshauri atakayekusaidia kutua mzigo wa fikira.

No comments: