Saturday, January 16, 2010

Je… Waijua homa?.... sehemu ya kwanza


Homa hutokea pale joto la mwili linapopanda. Kitaalamu joto la mwili hupanda pale linapozidi nyuzi joto 37 au Farenheit 98.6 kwa kipimo kinachokuliwa mdomoni au nyuzi joto 37.2 au Farenheit 99 kwa kipimo kinachochukuliwa katika makalio (rectal temperature). Hata hivyo kipimo cha wastani na joto la mwili huweza kupanda au kupungua kwa nyuzi joto 0.6 au Farenheit 1 kutoka Farenheit 98.5. Joto la miwli huweza kuongezeka kwa nyuzi joto 0.6 au Farenheit 1 wakati wa mchana. Kwa hivyo homa haichukuliwi kuwa ni hatari hadi pale joto la mwili llinapozidi nyuzi joto 38 au Farenheit 100.4. Homa inasaidia mwili kujilinda na bakteria na virusi ambavyo haviwezi kuishi katika joto kali. Kwa sababu hiyo, joto la chini kwa kawaida halitibiwi, hadi pale linapoambatana na dalili mbalimbali nyinginezo. Homa ni dalili mojawapo ya ugonjwa, na mara nyingi haizingatiwi hadi pale inapoandamana na dalili nyinginezo kama kukohoa, kuvimba koo, maumivu na kadhalika. Homa ya kufikia nyuzi joto 40 au Farenheit 104 inahitajia matibabu ya haraka, kwani isipotibiwa huweza kusababisha matatizo ya ubongo yanayopelekea kutapatapa usingizini kama vile kuota njozi au mawenge, pamoja na degedege hasa kwa watoto.
Themometa za dijitali zinaweza kutumika kupima joto kwa njia ya mdomoni, kwapani au katika makalio. Wataalamu wanashari ni bora isitumiwe themometa ya glasi yenye mekyuri, na ni bora wazazi wasiwe na themometa za aina hizo majumbani ili kuzuia hatari ya mada hiyo hatari yenye sumu.
Ni muhimu kutambua kuwa kipimo cha joto kinachochukuliwa kwapani si sahihi sana kikilinganishwa na kile cha mdomoni na makalioni (rectal) na kwa kawaida huwa pungufu kwa nyuzi joto moja kuliko kile kinachochukuliwa mdomoni.
….makala hii inaendelea.

No comments: