Wednesday, January 6, 2010

Namna ya kujikinga na Ugonjwa wa Kifua Kikuu… sehemu ya mwisho



Kuna njia mbalimbali zakujikinga na ugonjwa wa Kifua kikuu au TB ambazo ni:
 Kujikinga na Kifua Kikuu kunaanzia kabla ya mtu kupatwa na ugonjwa huo kwa watu wa kaiwada, ambapo kinga ya kuulinda mwili na ugonjwa huo hutolewa kwa watoto wadogo baada ya kuzaliwa. Kinga hiyo ya Kifua kikuu huitwa BCG yenye maana ya ( Bacillus Calmette- Guerin (BCG).
 Kuwakinga watu wa familia za wale walio karibu na wanaouguwa ugonjwa wa Kifua Kikuu.
 Kuwakinga wale wenye vijidudu vya ugonjwa wa kifua kikuu mwilini mwao lakini bado dalili za ugonjwa huo hazijajitokeza.
 Kuwakinga wale waliokuwa katika hatari ya kupatwa ugonjwa wa Kifua Kikuu.
Dawa aina ya Isoniazid (INH) inaweza kutumika katika kuzuia Kifua Kikuu kwa wale waliokuwa na vijidudu vya Kifua Kikuu katika miili yao lakini bado dalili za ugonjwa huo hazijajitokeza. Huko nyuma dawa aina ya Rifampin ilikuwa ikitumika kuzuia TB lakini kwa wale ambao dawa ya Isoniazid haikuwafaa.
Ugonjwa wa Kifua Kikuu ni ugonjwa unaozuilika kwa kiasi kikubwa. Ili kuwazuia watu wasipate ugonjwa huo inapasa watu walioambukizwa ugonjwa huo wajulikane mapema, hasa wale wanaokabiliwa na hatari kubwa ya kuonyesha dalili ya ugonjwa huo katika siku za usoni. Dawa ya INH inatumiwa kwa kiasi kikubwa kuzuia watu wasipate ugonjwa wa TB ambao wanaishi karibu na wagonjwa wa Kifua Kikuu au wale wenye uhusiano na wagonjwa hao, au wale wenye vimelea vya Tubercle bacilli katika miili yao lakini bado hawajafikia katika hali ya kuwa na TB halisi. Dawa hiyo hupewa na kutumiwa kila siku kwa miezi 12 mfululizo.
Katika nchi zilizoendelea kama vile Marekani, watu wa makundi yafuatayo wanapaswa kupewa dawa za kujikinga, bila kujali umri wao, iwapo huko nyuma hawajawahi kutibiwa ugonjwa wa Kifua Kikuu.
1. Watu ambao wanaishi na kushirikiana na wale walioambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu. (zaidi ya hayo watoto, na vijana ambao kipimo cha PPD kimeonyesha kuwa hawana ugonjwa huo, lakini kwa miezi mitatu wamekuwa wakiishi au kuwa na wa karibu na wenye ugonjwa huo. Matibabu yanapaswa kuendelea hadi pale kipimo cha ngozi kitakapochukuliwa tena na majibu kuonyesha hawajaambukizwa ugonjwa huo.
2. Watu ambao kipimo cha ngozi cha Kifua kikuu kimeonyesha wana ugonjwa huo, pamoja na wale ambao picha yao ya X-ray inaonyesha wana ugonjwa wa TB ingawa bado hawajaonyesha dalili za ugonjwa huo. (Inactive TB).
3. Watu ambao kipimo cha ngozi cha kifua kikuu kimeonyesha wana ugonjwa huo lakini pia wanakabiliwa na hatari ya kuambukizwa magonjwa kama vile ya HIV, Kisukari au wale wanaotumia dawa aina ya Corticosteroid.
4. Waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi na wale wanaodaniwa kuwa wameambukizwa virusi vya HIV na ambao wakati wowote huko nyuma kipimo cha ngozi kiliwahi kuonyesha wameambukizwa ugonjwa huo, hata kama hawana dalili.
5. Wale wanaotumia madawa ya kulenya kwa njia ya kujitunga sindano, ambao vipimo vya ngozi vimeonyesha wameambukzwa ugonjwa huo, hata kama bado hawana dalili za ugonjwa huo.
Watu wafuatao pia wenye umri wa zaidi ya miaka 35, wanapaswa kupewa dawa za kuzuia kifua kikuu:
 Wale wanaoishi katika maeneo yenye maambukizo mengi ya TB.
 Watu ambao wanaishi katika mazingira magumu, wale ambao wana kipato cha chini na wanaishi katika maeneo yenye misongamano.
 Watu ambao wameishi kwa muda mrefu jela, majumba ya kulelea wazee na sehemu za watu wenye matatizo ya kiakili.
Inapaswa kujua kuwa:
o Wafanyakazi wa vitengo vya afya wambao mara kwa mara wanakutana na kuwashughulikiwa wagonjwa wa kifua kikuu wanapaswa kufanyiwa vipimo vya ngozi vya TB kila baada ya miezi 6.
o Wagonjwa wenye kifua kikuu wanapaswa kufundishwa kuziba midomo yao na pua pale wanapokohoa au kupiga chafya.
o Wagonjwa wenye Kifua Kikuu wanapaswa kutengwa na kuwekwa kwenye vyumba ambavyo hewa inabadilika kwa urahisi.
o Wazazi wahakikishe kuwa watoto wao wanapatiwa kinga ya kifua kikuu katika wakati unaotakiwa.
'Daima tuzitunze afya zetu'

No comments: