Saturday, January 30, 2010

Chanjo inaweza kuwaokoa waathirika wa HIV wasife na TB


Wataalamu wamesema kuwa, wamepata chanjo inayoweza kuwasaidia wagonjwa wa TB ambao wameathirika na HIV. Chanjo hiyo inafanya kazi kwa kuupa nguvu mfumo wa kulinda mwili kwa wagonjwa ambao tayari waliwahi kupata chanjo ya BCG walipokuwa wadogo. Utafiti huo uliochapisha katika Jarida la AIDS umebainisha kuwa, wagonjwa wengi wenye Kifua Kikuu ambao walipewa chanjo hiyo walionekana kupata nafuu. Wataalamu hao kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Dartmouth cha Marekani wamejaribu chanjo hiyo kwa waathirika wa Ukimwi elfu mbili nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka 7 na kuthibitisha kwamba, ugonjwa wa TB uliweza kupunguzwa kwa asilimia 39 kwa wale waliopatiwa chanjo hiyo. Wataalamu hao wanasema kuwa, chanjo hiyo inaweza kuwa chaguo lisilogharimu fedha nyingi hasa kwa nchi zinazojitahidi kutafuta fedha kwa ajili ya kununua madawa ya kupambana na HIV. Chanjo hiyo inasemekana kuwa na uwezo zaidi wa kumlinda mgonjwa asipate kifua kikuu, pia inaweza kumlinda mgonjwa kwa miaka kadhaa. Profesa Ford von Reyn aliongoza utafiti huo, amesema hiyo ni hatua kubwa na kushauri kuwa, pale watu wanapogunduliwa wameathirika na HIV wanaweza kupewa chanjo hiyo, kabla hata ya kuanza kutumia vidonge vya kuongeza maisha ya antriretroviral. Reyn aidha amesema kwamba hii ni mara ya kwanza wamefanikiwa kupata chanjo ambayo ina athari kubwa katika kuzuia magonjwa yanayosababishwa na vijidudu vinavyowashambulua wagonjwa pale wanapokuwa na UKIMWI.
Ni muhimu kujua kuwa, Kifua Kikuu ni tatizo kubwa kwa watu wanaoishi na virusi vya HIV barani Afrika. Ugonjwa wa Tb unaongoza katika kuwasababishia vifo waathiriwa wa Ukimwi. Shirika la Afya Duniani linakadiria watu milioni 10 wana ugonjwa wa Kifua Kikuu pamoja na UKIMWI duniani, ambapo wengi wao wanaishi katika nchi za Afrika zilizoko chini ya Jangwa la Sahara. TB inaua kila mgonjwa mmoja kati ya watatu ambao wana UKIMWI.

No comments: